Hakika, aliyewakusanya pamoja waumini hawa katika mji huu si mwingine bali ni Mtume wetu Mtwaharifu Muhammad Mustafa (saww) – yule ambaye Allah amemuelezea kama Rehma kwa walimwengu wote: وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا رَحْمَةً لِّلْعَالَمِينَ “Wala hatukukutuma isipokuwa uwe rehema kwa walimwengu.” (Al-Anbiyaa: 107)

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt as -ABNA- Sherehe za Maulid zilizofanyika mjini Nakuru – Kenya zimeendelea kung’ara na kuleta faraja kubwa kwa waumini kutoka pembe mbalimbali za Kenya na Tanzania. Wingi wa watu, umoja wao na mapenzi yao kwa Mtume Muhammad (saww) vilidhihirika wazi katika mahudhurio yao mazuri na adabu zao njema wakati wa kusikiliza mafunzo na malezi ya kiroho yanayotokana na mwanga wa Mtume (saww).

Hakika, aliyewakusanya pamoja waumini hawa katika mji huu si mwingine bali ni Mtume wetu Mtwaharifu Muhammad Mustafa (saww) – yule ambaye Allah amemuelezea kama Rehma kwa walimwengu wote:
﴿ وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا رَحْمَةً لِّلْعَالَمِينَ ﴾
“Wala hatukukutuma isipokuwa uwe rehema kwa walimwengu.” (Al-Anbiyaa: 107)
Mwongozo na baraka za Mtume (saww) ndizo zilizoleta nyoyo hizo pamoja katika jiji la Nakuru, zikawakutanisha waumini wa tamaduni, mataifa na mikoa tofauti chini ya kivuli kimoja cha mapenzi yake tukufu. Tukio hilo limekuwa mfano hai wa kauli ya Mtume (saww):
“Waumini katika kupendana kwao, kuhurumiana kwao na kuoneana kwao fadhili ni kama mwili mmoja.”
Katika mazingira hayo yenye nuru, waumini walijengewa matumaini makubwa ya kupata Shafaa ya Mtume Muhammad (saww) Siku ya Kiyama, kwani yeye mwenyewe amesema:
“Shafaa yangu ni kwa ajili ya wenye kufanya madhambi miongoni mwa Ummah wangu.”

Na Qur’ani inatuonyesha daraja la Mtume (saww) katika neema ya uombezi:
﴿ وَلَسَوْفَ يُعْطِيكَ رَبُّكَ فَتَرْضَى ﴾
“Na Mola wako atakupa mpaka uridhike.” (Ad-Duhaa: 5)
Kwa hivyo, safari ya waumini hawa kuelekea Nakuru haikuwa tu safari ya kimwili, bali ilikuwa ni mwito wa kiroho uliochochewa na mapenzi na ikhlasi kwa Mtume wa Rehma na Amani (saww).
Waliokusanyika pamoja waliondoka wakiwa na faraja, elimu, mawaidha na muamko mpya wa kuendelea kuishi kwa mwanga wa Sunna, maadili na upendo alioufunza Mtume (saww). Hafla ya ndoa iliyofanyika sambamba na Maulid imezidisha baraka, ikithibitisha kwamba Maulid si tu kumbukumbu ya kuzaliwa kwake bali pia ni kutenda yale aliyoyapenda Mtume (saww) – umoja, ndoa, maadili, ikhlas na kuhuisha misingi ya familia bora.

Kwa pamoja, matukio hayo yote yameacha alama nzuri ya kiroho na kijamii, na yamewafanya waumini kuzungumza kwa sauti moja:
“Tunatarajia Shafaa ya Mtume wetu Muhammad (saww) Siku ya Kiyama – InshaAllah.”

Your Comment